SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA
2023-01-06 08:00:42| CRI

Naam msikilizaji kama ulivyosikia kipindi kilichopita tulizungumzia sana kuhusu haki za mtoto wa kike, na tulisikia watu wa ngazi mbalimbali wakizungumzia ukatili wanaokumbana nao watoto wa kike na wanawake. Pia tulisikia jinsi wanaharakati wanavyojitahidi kupambana na ukatili huu. Lakini ukatili wa kijinsia sio tu kupigwa, kubakwa ama kulawitiwa, ukatili wa kijinsia pia unahusisha na rushwa hususan rushwa ya ngono ambayo wanawake wanakumbana nayo katika maeneo mengi, iwe ni shuleni, vyuoni au hata maeneo ya kazi.

Novemba 26 hadi Desemba 10 kila mwaka ni Siku 16 za Kupambana na Ukatili wa Kijinsia. Katika kipindi hicho cha siku 16, shughuli mbalimbali za kutetea na kupinga ukatili wa kijinsia zinafanyika katika nchi mbalimbali duniani, huku mashirika ya kiraia na serikali katika nchi husika zikijitahidi kuendelea kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na pia kwa wanaume, katika maeneo ya shule, na pia katika mikutano ya hadhara. Wadau na watetezi wa haki za binadamu pia wako mbele katika kuhakikisha kuwa sauti za watoto wa kike na wanawake zinasikika, na kupinga kidhahiri vitendo vyovyote vya ukatili wa kijinsia. Hivyo basi, katika kipindi cha leo, tutaangazia ukatili dhidi ya watoto wa kike na wanawake, na nini kifanyike ili kutokomeza kabisa vitendo hivyo.