Watu 10 wauawa katika milipuko miwili ya mabomu katikati ya Somalia
2023-01-05 08:22:37| CRI

Watu 10 wameuawa na wengine saba kujeruhiwa katika milipuko miwili ya mabomu inayoshukiwa kutekelezwa na wapiganaji wa kundi la al-Shabaab katika mji wa Mahas, katikati ya Somalia mapema jana.

Mkuu wa Wilaya ya Mahas Mumin Mohamed Halane amesema, magari mawili yaliyotegwa mabomu yalilenga nyumba wanazoishi maofisa wa serikali wanaongoza mapambano dhidi ya ugaidi katika kanda ya Hiran, lakini hawakuwepo nyumbani wakati wa shambulizi hilo, na kwamba idadi kubwa ya watu waliofariki ni raia.

Hakuna kundi lililokiri kuhusika na shambulizi hilo, lakini tangu mwaka 2007, kundi la al-Shabaab limekuwa likifanya mashambulizi mabaya nchini Somalia dhidi ya maofisa wa serikali na askari wa kulinda amani kutoka Umoja wa Afrika.