Marais wa China na Turkmenistan wafanya mazungumzo mjini Beijing
2023-01-06 15:58:09| CRI

Rais Xi Jinping wa China amefanya mazungumzo na mwenzake wa Turkmenistan Serdar Berdimuhamedov leo hapa Beijing. Marais hao wawili wametangaza kuinua ngazi ya uhusiano kati ya nchi zao kuwa wenzi wa kimkakati wa pande zote.

Kwenye mazungumzo yao, rais Xi Jinping amesema China inapenda kushirikiana na Turkmenistan kuimarisha uhusiano katika sekta zote, na kuhimiza ujenzi wa jumuiya yenye hatma ya pamoja kati ya China na Turkmenistan ili kuendeleza zaidi uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Rais Xi amesisitiza kuwa China na Turkmenistan zote ni nchi zinazolinda amani, kutafuta maendeleo na kwenda sambamba kuhimiza mageuzi ya usimamizi wa dunia. Amesema China inaunga mkono ushirikiano wa kiujenzi kati ya Turkmenistan na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai SCO, na inapenda kutekeleza kwa vitendo utaratibu halisi wa pande nyingi, na kujenga jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja.

Kwa upande wake, rais Serdar Berdimuhamedov ameeleza kufurahia kufanya ziara nchini China katika siku ya maadhimisho ya 31 ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Turkmenistan na China, na kwamba nchi yake inapenda kuimarisha ushirikiano wa kunufaishana na China. Amesisitiza kuwa Turkmenistan inaunga mkono kithabiti juhudi za China za kulinda mamlaka na ukamilifu wa ardhi na kupinga vitendo vyovyote vya kujaribu kuifarakanisha China.

Baada ya mazungumzo yao, marais hao wawili walisaini na kutangaza Taarifa ya Pamoja ya Jamhuri ya Watu wa China na Turkmenistan, na pia kushuhudia kusainiwa kwa nyaraka za ushirikiano kuhusu “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, maendeleo ya kijani, uchumi wa kidigitali, afya, utamaduni, michezo, vyombo vya habari na gesi asilia.