Mamlaka ya Msumbiji yasema huenda mafuriko yataendelea kuyakumba majimbo ya kusini kutokana na mvua kubwa
2023-01-06 08:30:55| CRI

Ofisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji wa Msumbiji Agostinho Vilanculos amesema huenda mafuriko yataendelea kuzikumba wilaya kadhaa za Maputo na Gaza, majimbo ya kusini mwa nchi hiyo, kutokana na mvua kubwa inayoendela kunyesha nchini humo na nchi jirani.

Vilanculos amesema mabwawa makuu ya nchi jirani ya Afrika Kusini na Eswatini kwa sasa yamefikia uwezo wake wa kuhifadhi maji, huku maji yakiendelea kutiririka kwenye Mito ya Umbeluze, Maputo, Inkomati na Limpopo nchini Msumbiji, na kutoa wito wa kuhamishwa kwa haraka kwa jamii zinazoishi au kufanya shughuli za kilimo kwenye ukingo wa mito hiyo.

Ofisa huyo ameongeza kuwa takriban watu milioni 2.2 huenda wataathiriwa na mafuriko kote nchini humo wakati wa msimu wa mvua wa sasa ulioanzia mwezi Oktoba hadi Machi.