UM watoa wito wa kusimamisha mvutano kufuatia ziara ya waziri wa Israel katika msikiti wa Al-Aqsa
2023-01-06 08:29:49| CRI

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya Mashariki ya Kati, Asia na Pasific Khaled Khiari ametoa wito wa kupunguza mvutano kufuatia ziara ya Waziri wa Ulinzi wa Israel Itamar Ben-Gvir katika uwanja wa Msikiti wa Al-Aqsa ulioko Yerusalem Mashariki.

Amesema kama ilivyoonekana mara kadhaa katika siku zilizopita, hali katika maeneo matakatifu ya Yerusalem ni tete, na shughuli yoyote ama mvutano katika maeneo hayo inaweza kusababisha vurugu katika eneo lote la Palestina linalokaliwa, Israel, na katika maeneo mengine ya kanda hiyo.

Bw. Khiari amerejea tena wito uliotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa pande zote husika kujizuia kuchukua hatua zinazoweza kuongeza mvutano katika maeneo matakatifu, na kudumisha hali kama ilivyokuwa awali.