Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU atoa salamu za rambirambi kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea Senegal
2023-01-09 08:49:00| CRI

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Bw. Moussa Faki Mahamat jana alitoa salamu za rambirambi kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyosababisha vifo na majeruhi ya watu zaidi ya 40 nchini Senegal. Alitoa salamu hizo kwa familia za wafiwa wa ajali hiyo kupitia mtandao wa kijamii, na kuwatakia majeruhi wapone haraka.

Taarifa iliyotolewa na mamlaka husika ya huko, inasema ajali hiyo imetokea baada ya mabasi mawili kugongana katika eneo la Kaffrine, katikati ya nchi hiyo.

Rais Macky Sall wa Senegal ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kufuatia ajali hiyo, pia amesema baraza la mawaziri la nchi hiyo litafanya mkutano ili kuchukua hatua madhubuti kuhusu usalama barabarani na usafiri wa umma.