Katibu mkuu wa UM akaribisha kuanza kwa kipindi cha mwisho cha mpito wa kisiasa nchini Sudan
2023-01-10 10:03:44| CRI

Msemaji wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres amekaribisha kuanza kwa kipindi cha mwisho katika mchakato wa mpito wa kisiasa nchini Sudan.

Bw. Dujarric amesema hatua ya kuanza kwa kipindi hicho iliyohimizwa katika msingi wa makubaliano ya mfumo wa kisiasa yaliyosainiwa tarehe 5 Desemba mwaka jana, ni hatua nyingine muhimu kuelekea kufikia matarajio ya watu wa Sudan kwa demokrasia, amani na maendeleo endelevu. Amesema Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na mashirika mengine husika yataendelea kuunga mkono mchakato huo na kusaidia kufikiwa kwa makubaliano ya mwisho ya kisiasa katika wiki zijazo.

Ameongeza kuwa ili kupata suluhu ya kudumu, ni muhimu kujumuisha nguvu ya umma nchini Sudan. Pia alisisitiza umuhimu wa uungaji mkono wa kimataifa ulio thabiti na ulioratibiwa katika mchakato huo chini ya mfumo wa Utaratibu wa Pande Tatu.