Shirika la Ndege la Ethiopia kurejesha safari za China kama ilivyokuwa kabla ya janga la Corona
2023-01-11 09:38:18| CRI

Shirika la Ndege la Ethiopia limesema linapanga kurejesha safari za ndege za kwenda China kwenye hali ya zamani ilivyokuwa kabla ya janga la COVID-19.

Shirika hilo limesema litaongeza safari za ndege za kwenda China kuanzia tarehe 6 Februari. Mpango huo ni pamoja na kuendesha safari za kila siku kwenda Guangzhou, na kuongeza safari za Beijing na Shanghai hadi nne kila wiki, na kuendelea na safari tatu za mji wa Chengdu kila wiki. Kuaniza tarehe mosi Machi, safari zake za ndege zitapangwa kurejeshwa kwenye kiwango sawa na kile cha wakati kabla ya janga la COVID-19, yaani safari za Beijing na Shanghai kila siku, na safari nne kwenda Guangzhou na Chengdu kila wiki.

Mkuu wa Shirika la Ndege la Ethiopia Bw. Mesfin Tasew amepongeza mpango huo akisisitiza kuwa China ni moja ya masoko makubwa zaidi kwa shirika hilo nje ya bara la Afrika huku akitarajia ongezeko hilo la safari za ndege litasaidia kuziweka karibu zaidi nchi za Afrika na China.