SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA (2)
2023-01-11 14:12:04| CRI

Naam msikilizaji kama tulivyokuahidi kipindi kilichopita kwamba tutaendelea kuangazia suala hili la ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wa kike. Katika kipindi kilichopita uliweza kumsikia Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum, Dkt. Dorothy Gwajima akituasa kwamba, tunapaswa kuwauliza watoto wetu, nani amewashika wapi, na nani amewapa zawadi gani, nani amewaambia wakutane sehemu iliyojificha? Maswali haya tunapaswa kuwauliza watoto wetu. Lakini zaidi pia, tuwe karibu na watoto wetu, maana ni mengi wanayokumbana nayo wakiwa njiani kwenda na kurudi kutoka shuleni. Ni hivi karibuni tu kulikuwa na taarifa kuhusu mtoto wa shule kufanyiwa ukatili na dereva wa basi la shule. Matukio kama haya kwa kweli yanasikitisha sana, na ni jukumu la jamii nzima kushirikiana ili kuweza kukomesha kabisa vitendo hivyo.

Suala lingine ambalo pia linapaswa kutupiwa macho ni udhalilishaji wa wanawake katika sehemu za kazi. Unaweza kuona mfanyakazi mwanamke analipwa mshahara mdogo kuliko mwanaume, na kazi wanazofanya ni sawa, au hata mwanamke anafanya kazi zaidi kwa maana inabidi aonyeshe uwezo wake na kwamba anamudu kazi hiyo. Hivi karibuni nilisoma habari moja kuhusu mwigizaji maarufu wa Bollywood na Hollywood Priyanka Chopra Jones aliweka wazi kuwa, malipo yake katika kipindi alichoigiza Bollywood yalikuwa ni asilimia 10 ya mwigizaji mwenzake wa kiume, na alipata malipo kamili sawa na mwigizaji wa kiume baada ya kuigiza katika filamu moja ya Hollywood. Mambo kama haya kwa kweli yanatakiwa kufuatiliwa na wahusika ili kuondoa pengo hili ambalo linatokana na tu jinsia. Basi msikilizaji, kipindi cha leo tutaendelea kuzungumzia ukatili wa kijinsia, hususan kwa wanawake na watoto wa kike.