Viongozi wa Sudan Kusini na Sudan wakubaliana kuimarisha usalama na biashara
2023-01-13 09:36:06| CRI

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amekutana na mwenzake wa Sudan Abdel Fattah Al-Burhan, wakijadili njia za kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na usalama kati ya nchi zao.

Kwa mujibu wa naibu waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Bw. Mayen Dut Wol, viongozi hao wawili wamekutana mjini Juba, wakisisitiza tena ahadi ya kuhakikisha uhuru wa kusafiri, ukazi, upatikanaji wa mali na ajira kwa raia wote wa nchi zote mbili.

Bw. Dut amesema, Rais Salva Kiir na Bw. Al-Burhan ambaye ni mwenyekiti wa baraza la mamlaka la mpito la Sudan, wamejadili masuala makuu kutoka utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano yaliyosainiwa mwaka 2012 hadi biashara na usalama katika maeneo ya mipakani kati ya nchi hizo mbili za jirani.

Viongozi hao pia wamesisitiza umuhimu wa kuhakikisha utulivu na usalama mipakani, ili kuhimiza amani na ustawi kwa nchi zote mbili. Pia wamekubaliana kuzindua kikosi cha pamoja cha usalama ili kuzuia upatikanaji wa silaha haramu na kupambana na vikosi na shughuli hasi katika maeneo ya mipakani.