Rais wa Misri atoa wito wa kuimarisha uratibu na China katika masuala ya kimataifa na ya kikanda
2023-01-16 14:13:56| CRI

Rais Abdel-Fattah al-Sisi wa Misri ametoa wito wa kuimarishwa uratibu kati ya Misri na China katika masuala ya kimataifa na kikanda, pamoja na kuhimiza zaidi ushirikiano wa nchi za kiarabu na China na pia Afrika na China.

Sisi alisema hayo jana Jumapili katika mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang aliyeko ziarani mjini Cairo, mji mkuu wa Misri.

Sisi alisema China ni nchi kubwa na maendeleo yake hayawezi kuzuiliwa, na kwamba urafiki kati ya Misri na China umekuwa imara “usioweza kuvunjika” katika historia.

Misri itaendelea kushikilia kithabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja na kupinga kwa uthabiti uingiliaji wowote wa mambo ya ndani ya China unaofanywa na nchi za nje.

Akipongeza matokeo mazuri ambayo Misri na China zimepata katika kuendeleza kwa pamoja Mpango wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, Sisi alisema makampuni ya China yanakaribishwa kuwekeza na kuanzisha biashara nchini Misri.

Qin kwa upande wake alisema China na Misri zimesaidiana na kujenga urafiki wa dhati katika kutafuta maendeleo, kuhimiza amani na kulinda haki. China inaunga mkono Misri kufuata njia ya maendeleo inayolingana na hali yake ya kitaifa na kulinda mamlaka, usalama na maslahi yake ya maendeleo. Ameongeza kuwa anatazamia kuoanisha kwa karibu mikakati ya maendeleo ya nchi hizo mbili, kuharakisha ujenzi wa miradi muhimu ya ushirikiano, na kupata matokeo zaidi katika ujenzi wa Ukanda Mmoja, Njia Moja pamoja na utekelezaji wa matokeo ya Mkutano wa wakuu wa China na nchi za Kiarabu nchini Misri.