Waziri wa mambo ya nje wa China afanya mazungumzo na katibu mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
2023-01-16 13:01:40| cri

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Ahmed Abou Gheit wamekubaliana kuongeza kasi ya utekelezaji wa matokeo ya mkutano wa kwanza kati ya China na nchi za kiarabu.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika jana jumapili mjini Cairo, Misri, Bw. Gheit amesema nchi za kiarabu ziko tayari kuongeza mawasiliano na China katika utekelezaji wa mapendekezo manane muhimu yaliyofikiwa katika Mkutano wa kwanza kati ya China na Nchi za Kiarabu, pia ameishukuru China kwa kudumisha haki katika uwanja wa kimataifa, kuunga mkono maendeleo ya nchi za kiarabu na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, na msaada wake kwa nchi za kiarabu katika mapambano dhidi ya janga la COVID-19.

Kwa upande wake, Bw. Qin Gang amesema China iko tayari kushirikiana na nchi za kiarabu kutekeleza matokeo ya Mkutano wa kwanza kati ya China na Nchi za Kiarabu katika moyo wa urafiki kati ya pande hizo mbili na kuongeza kasi ya utekelezaji wa makubaliano manane ya ushirikiano yaliyopendekezwa katika mkutano huo ili kuzinufaisha pande zote mbili. Pia, Bw. Qin ametoa wito kwa pande hizo kuimarisha ujenzi wa mikakati chini ya mfumo wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Nchi za Kiarabu ili kuongeza ngazi ya ushirikiano wa pande mbili.