Miili 68 yapatikana kwenye ajali ya ndege ya Nepal
2023-01-16 11:55:59| CRI

Afisa wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Nepal (CAAN) Jagannath Niroula amesema jumla ya miili 68 imepatikana baada ya ndege iliyobeba watu 72 kupata ajali Jumapili katika mkoa wa Pokhara katikati mwa Nepal.

Ndege ya ATR-72 kutoka shirika la ndege la Yeti iliondoka Kathmandu saa 4:30 asubuhi kwa saa za huko na kupoteza mawasiliano na mnara wa kuongozea ndege saa 4:50, hata hivyo kwa mujibu wa CAAN hali ya hewa haikuwa sababu ya ajali hiyo, kwani ilikuwa nzuri na rubani hakuripoti matatizo yoyote ya kiufundi.

Mkuu wa polisi wa wilaya ya Kaski ilipo Pokhara amesema miili imepatikana katika eneo la ajali katika korongo la Mto Seti ambalo lina kina cha zaidi ya mita 200. Naye msemaji wa jeshi la Nepal Brigedia Mkuu Krishna Prasad Bhandari amesema miili mingi haikuweza kutambuliwa na asilimia 80 ya ndege imeungua moto.

Juhudi za kuwatafuta watu wengine wanne bado zinaendelea. Abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo 15 ni wageni wakiwemo Wahindi watano, Warussia wanne, Wakorea Kusini wawili, Muaustralia mmoja, Muireland mmoja, Muargentina mmoja na Mfaransa mmoja.