Watu wanane wafariki katika shambulizi la bomu Somalia linalodaiwa kufanywa na kundi la Al-Shabaab
2023-01-16 13:03:09| cri

Polisi nchini Somalia wamesema watu wanane wameuawa katika shambulizi la bomu lililotegwa kando ya barabara linalodaiwa kufanywa na kundi Al-Shabaab katikati mwa Somalia, ambako mashambulizi makubwa yanaendelea ili kukomboa eneo hilo kutoka kwa wapiganaji wa kundi hili.

Shambulizi hilo lilitokea Jumamosi alasiri huko Buloburde, mji ulio katika wilaya ya Hiran ambapo vikosi vya serikali na wanamgambo wa koo wamekuwa wakipambana na waasi wenye uhusiano na Al-Qaeda tangu katikati ya mwaka jana. Kamanda wa polisi wa eneo hilo Abdullahi Mohamud amesema mshambuliaji alilipua gari lililokuwa limebeba mabomu karibu na jengo la utawala.

Katika tukio lingine polisi wamesema bomu lililotegwa ndani ya gari lililipuka huko Jalalaqsi, mji mwingine wa Hiran, lakini ni mshambuliaji pekee aliyekufa. Shambulio la pili lilizimwa na mshukiwa alikamatwa wakati akijaribu kulikimbia na gari lililokuwa na milipuko. Kundi la Al-Shabaab limesema linahusika na matukio yote hayo matatu.