Xi atoa salamu za mwaka mpya wa jadi wa China kwa Wachina wote
2023-01-19 09:32:48| CRI

Rais Xi Jinping wa China Jumatano wakati alipoongea na taifa kupitia njia ya video kabla ya Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China, alitoa salamu za mwaka mpya wa jadi wa China kwa Wachina wote, na kuwatakia afya njema na maisha ya furaha katika mwaka wa Sungura, huku akieleza matarajio yake kwamba nchi itakuwa na ustawi.

Rais Xi, aliongea na watumishi wa afya hospitalini, wazee kwenye nyumba za kutunza wazee, wafanyakazi wa sekta ya mafuta, wasafiri na wafanyakazi wa kituo cha reli ya kasi, wachuuzi na wateja katika soko la jumla, na watu wa vijiji vya makabila madogo.

Rais Xi pia amegusia suala la kupambana na UVIKO-19 akisema mwangaza wa matumaini upo mbele. Amefafanua kuwa nchi imefanya maamuzi sahihi kupambana na virusi vya Corona kwa kuchukua hatua kali katika miaka karibu mitatu, na kuiwezesha China kuhimili duru kadhaa za milipuko ya virusi vya Corona. Hivyo ametaka kuwepo na juhudi za kuongeza rasilimali za matibabu na usambazaji wa huduma za matibabu na dawa, na kujiandaa kwa matibabu hasa kwa wagonjwa wenye dalili kali.

Mbali na hayo rais Xi ametoa wito wa kufanikisha zaidi ustawishaji wa vijiji, na kuwataka wanakijiji wajitahidi kwa ajili ya ustawi wa pamoja na kufanya maisha yao yawe mazuri.