Utekelezaji wa AfCFTA kukuza biashara ya ndani ya Afrika
2023-01-19 09:29:53| CRI

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa barani Afrika (ECA) Bw. Antonio Pedro amesema kuwa utekelezaji wa makubaliano ya Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA) unapaswa kuharakishwa kwani eneo hilo litakuza biashara ya ndani ya Afrika na kuharakisha ukuaji wa viwanda.

Taarifa iliyotolewa na UNECA ilimkariri Pedro akisema kuwa wakati ahadi ya AfCFTA ni kubwa, ahadi hiyo inaweza kutekelezwa iwapo tu makubaliano hayo yatatekelezwa kwa ufanisi. Kutekeleza Makubaliano ya AfCFTA na kusaidia uchumi wa Afrika, hasa Nchi zilizo nyuma zaidi kimaendeleo (LDCs), haikuwa kazi ndogo.

Ameongeza kuwa AfCFTA imetoa ahadi ya kusaidia Nchi zilizo nyuma zaidi kimaendeleo kufufuka na kuongeza kasi ya ukuaji, akitolea mfano tathmini ya hivi karibuni ya UNECA ambayo inaonyesha mafanikio ya utekelezaji wa AfCFTA utaleta matokeo mazuri kwa Pato la Taifa, biashara na ustawi wa Afrika.

Aidha amesema kwa makubaliano ya AfCFTA, eneo la biashara huria barani Afrika, kutafanya biashara kukua kwa asilimia 34 hadi kufikia mwaka 2045 kuliko ambavyo ingekuwa bila kuwepo kwa eneo hilo.