Makamu wa Rais wa Tanzania aamuru kukamatwa kwa polisi wasio waaminifu kwa kuharibu mradi wa reli
2023-01-19 09:31:14| CRI

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameliamuru jeshi la ulinzi wa taifa na mashirika ya kiusalama kuwasaka na kuwakamata maafisa wa polisi wasio waaminifu ambao wameshirikiana na wananchi kuharibu miundombinu ya mradi wa reli ya kisasa ya SGR.

Dkt. Mpango ametoa amri hiyo wakati akizindua ujenzi wa reli ya SGR ya Tabora hadi Isaka yenye urefu wa kilomita 165 katika stesheni ya reli mkoani Shinyanga, kaskazini mwa Tanzania. Hadi sasa polisi wamewakamata watu wengi wanaohusishwa na uharibifu wa miundo mbinu ya mradi wa SGR ikiwemo kuiba mafuta, saruji na vyuma vya reli. Dkt Mpango ameongeza kuwa waharibifu hao ni pamoja na madereva na waendeshaji wa mashine kwenye mradi huo pamoja na watu wanaoishi karibu na maeneo ya mradi ambao wanalindwa na maafisa wa polisi wasio waaminifu.