Elimu kwa mtoto wa kike
2023-02-06 08:20:07| CRI

Suala la elimu kwa mtoto wa kike limekuwa likijadiliwa kwa kina na kwa upana wake kwa muda mrefu, lakini bado mtoto wa kike anakumbwa na maswahibu mengi katika kutafuta elimu. Baadhi ya makabila, ama mila na desturi zinapinga mtoto wa kike kupata elimu, kwa madai kuwa, mtoto wa kike ataolewa na kwenda kwenye familia ya mume wake, hivyo hatakuwa msaada wowote kwa familia yake.

Lakini ukweli ni kwamba, mwanamke mara nyingi ndio amekuwa msaada mkubwa kwa familia yake na ya mume wake, mwanamke amekuwa akitafuta mbinu na njia za kuendeleza familia yake, na kutimiza mahitaji ya familia pale ambapo mwanaume ama mume ama mtoto wa kiume katika familia amekuwa akishindwa kutimiza wajibu wake. Kuna msemo kuwa, unapomwelimisha mtoto wa kike, unaelimisha jamii nzima, hivyo elimu kwa mtoto wa kike ni kitu cha muhimu sana, kwani atakuwa msaada mkubwa si kwa jamii yake tu, bali hata kwa taifa.

Lakini mtoto huyu wa kike anakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kusaka elimu, kuna udhalilishaji wa kijinsia, ukatili wa kingono, kubakwa, mimba za utotoni, kuonekana ni dhaifu kuliko mtoto wa kiume, na changamoto nyingine nyingi. Katika kipindi cha leo, tutazungumzia umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike pamoja na mwanamke.