Makamu wa Rais wa Tanzania atoa wito wa kulinda vyanzo vya maji ya Ziwa Victoria
2023-01-20 08:50:30| CRI

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa wito wa kulinda vyanzo vya maji yanayoingia ziwa Victoria, ambalo ni moja ya maziwa makubwa ya maji baridi duniani.

Dkt. Mpango ametoa wito huo muda mfupi tu kabla ya kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya kuanza mradi unaogharimu Shilingi bilioni 24.4 (sawa na dola milioni 10.4 za Marekani), ambao utachukua maji kutoka Ziwa Victoria na kuyasambaza katika miji ya Tinde na Shelui mkoani Shinyanga. Amesema kupungua kwa kiwango cha maji katika Ziwa Victoria kutaleta matokeo mabaya kwa binadamu, hivyo amezitaka mamlaka za maji nchini humo kutunga mikakati inayolenga kuhifadhi maji, ikiwemo kuvuna maji ya mvua ili kutumika wakati wa uhaba wa maji.

Likiwa na eneo la kilomita za mraba 68,800, Ziwa Victoria linatumiwa na nchi tatu zikiwemo Tanzania, Kenya na Uganda.