Mtu mmoja ajeruhiwa katika shambulizi dhidi ya kituo cha msaada nchini Sudan Kusini
2023-01-24 17:40:57| CRI

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema, mtu mmoja amejeruhiwa na vifaa kadhaa kuibiwa katika shambulizi dhidi ya kituo kimoja cha msaada huko Pibor, mashariki mwa Sudan Kusini ambapo mfanyakazi mmoja wa kituo hicho amejeruhiwa.

Amesema Kaimu Mratibu Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Bw. Peter Van der Auweraert amelaani vikali shambulizi hilo lililotokea Jumatano iliyopita.

Bw. Dujarric amesema, hilo ni shambulizi la tatu ndani ya mwezi huu baada ya mashambulizi mengine mawili kutokea katika eneo la Abyei na jimbo la Jonglei, ambapo washambuliaji walilenga mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) wakitafuta pesa taslimu na mali nyinginezo.

Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imesema, mashambulizi hayo yameathiri jamii zilizo hatarini kwa kuwa yamezuia usambazaji wa vifaa vya mahitaji dharura kwa ajili ya maisha ya watu.