DRC na Rwanda zalaumiana kutokana na shambulizi dhidi ya ndege ya kivita
2023-01-25 17:28:01| CRI

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC na Rwanda zimetupiana lawama baada ya ndege ya kivita aina ya Sukhoi-25 kutoka DRC kushambuliwa wakati ikitua, ukiwa ni mzozo mpya kati ya nchi hizo mbili jirani ambazo uhusiano wao umedorora kutokana na uasi.

Msemaji wa serikali ya DRC Bw. Patrick Muyaya ametoa taarifa akilaani shambulizi hilo na kukanusha shutuma za Rwanda kwamba ndege hiyo ilikuwa katika eneo la anga ya Rwanda.

Amesema, shambulizi la Rwanda lililenga ndege ya DRC iliyokuwa ikiruka juu ya eneo la DRC. Na amekanusha kuwa haikupita eneo la anga ya Rwanda kwa njia yoyote ile, akiongeza kuwa tukio hilo lilitokea saa kumi na moja jioni kwa saa za Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini na kwamba ilitua bila ya uharibifu mkubwa.

Mapema Jumanne, Rwanda ilitoa lawama dhidi ya ndege ya kivita ya DRC kuvamia eneo lake la anga kwa mara ya tatu, jambo ambalo limeifanya Kigali kuchukua hatua za kujilinda. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya msemaji wa serikali, Rwanda iliitaka DRC kuacha kufanya uvamizi kama huo.