Mjumbe wa China atoa wito kwa pande zote za Haiti kuendelea na mazungumzo jumuishi
2023-01-25 17:29:02| CRI

Mwakilishi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa Bw. Zhang Jun ametoa hotuba kwenye mkutano wa wazi wa Baraza la Usalama kuhusu Haiti, na kuzitaka pande zote nchini Haiti kuendelea kufanya mazungumzo jumuishi na kuongeza hali ya udharura katika mashauriano ya kisiasa.

Bw. Zhang amefahamisha kuwa katika mwaka uliopita hali haijatengemaa. Kuna ombwe la mamlaka ya kisiasa na ghasia za magenge zilizokithiri, kama milima miwili inayowaelemea watu wa Haiti. Mgogoro wa uhalali wa kisiasa ndio mzozo wa kimsingi zaidi wa Haiti.

Bw. Zhang amesema kuwa pande zote za Haiti zinapaswa kukubaliana juu ya mpango wa mpito unaokubalika kwa ujumla, unaoaminika na unaoweza kutekelezwa ili kuweka mazingira ya kufanyika kwa uchaguzi ulio huru na wa haki mapema. Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Haiti inapaswa kujenga jukwaa kwa ajili ya vyama vya kisiasa na makundi yote nchini Haiti kufanya mazungumzo, na kwa msingi wa kuheshimu uchaguzi wa watu wa Haiti, kuongeza jitihada za kukuza mchakato wa kisiasa unaoongozwa na unaomilikiwa na watu wa Haiti.