Awamu ya kwanza ya mradi wa reli ya umeme inayojengwa na China yafunguliwa nchini Nigeria
2023-01-25 17:25:39| CRI

Awamu ya kwanza ya mradi wa reli ya umeme inayojengwa na China katika jimbo la Lagos nchini Nigeria umefunguliwa rasmi kwa umma Jumanne.

Ukitekelezwa na kampuni ya Uhandisi ya China CCECC tangu 2010, njia iliyokamilika ya reli ya Lagos (LRMT) ina urefu wa kilomita 13 na ina vituo vitano. Reli hiyo ni ya kwanza kuvuka Okokomaiko, eneo ambalo lina watu wengi katika sehemu ya magharibi ya Lagos, na Marina, wilaya ya kibiashara katika kisiwa cha Lagos.

Akiongea kwenye tafrija iliyoandaliwa na serikali ya jimbo la Lagos kabla ya sherehe ya uzinduzi, rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ameelezea mradi huo kama wa kihistoria, akisema reli hiyo itapunguza msongamano barabarani na uchafuzi wa hewa, pamoja na kuboresha maisha ya wenyeji.

Naye Balozi wa China nchini Nigeria, Cui Jianchun, amesema kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi kunaonesha uhusiano wa maelewano kati ya China na Nigeria.