EAC yazindua tume ya uhakiki ili kutathmini utayari wa Somalia wa kujiunga na jumuiya
2023-01-26 17:26:07| cri

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Jumatano ilizindua rasmi tume ya uhakiki ili kutathmini utayari wa Somalia wa kujiunga na Jumuiya hiyo yenye wanachama saba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na makao makuu ya EAC mjini Arusha, tume ya uhakiki yenye wataalamu kutoka nchi wanachama wa jumuiya hiyo imekwenda nchini Somalia kuanzia jana Januari 25 na itakuwepo huko hadi Februari 3, ili kuangalia kiwango cha kulingana na vigezo vya kukaribisha nchi za nje, kama ilivyo kwenye mkataba wa kuanzisha EAC.

Akiongea wakati wa uzinduzi, Katibu Mkuu wa EAC Peter Mathuki amesema timu hiyo ambayo ipo Mogadishu, Somalia itashughulikia masuala husika ili kuhakikisha kwamba uhakiki unakamilika na ripoti ya utayari inamalizika kwa wakati ili kuwasilishwa katika Baraza la Mawaziri la EAC.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia na Ushirikiano wa Kimataifa Abshir Omar Jama ameeleza matumaini yake kwa timu hiyo na kusema kama wakiwa wanachama kamili wa EAC, Somalia itanufaika pakubwa kwasababu watu watakuwa wakisafiri kwa uhuru kutoka Somalia na nchi nyingine bila viza.