Uchumi wa dunia watarajiwa kukua kwa asilimia 1.9 mwaka 2023
2023-01-26 17:44:08| CRI

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Hali ya Uchumi na Matarajio ya mwaka 2023 ilisema ukuaji wa uchumi wa dunia unatarajiwa kushuka kutoka asilimia 3.0 ya mwaka 2022 hadi asilimia 1.9 ya mwaka 2023, na kuashiria moja ya viwango vya chini zaidi vya ukuaji katika miongo ya hivi karibuni.

Ripoti hiyo pia ilisema uchumi wa dunia unatarajiwa kukua polepole hadi asilimia 2.7 mwaka 2024, huku baadhi ya changamoto za uchumi mkuu zikitarajiwa kuanza kupungua mwaka ujao.

Wakati kukiwa na mfumuko mkubwa wa bei, sera kali za sarafu na kuongezeka kwa sintofahamu, kushuka kwa sasa kumepunguza kasi ya kufufua uchumi kutoka kwenye janga la COVID-19, na kutishia nchi zilizoendelea na zinazoendelea kwa pamoja kuingia kwenye hali ya kudidimia.

Ripoti hiyo ilisema kasi ya ukuaji ilidhoofika kwa kiasi kikubwa nchini Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine zilizoendelea mwaka 2022, na kuathiri vibaya uchumi wa sehemu nyingine za dunia kupitia njia mbalimbali.