Shirika la Ndege KLM laziomba radhi Tanzania na Kenya kwa madai ya kuwepo machafuko katika nchi hizo
2023-01-30 15:33:37| cri

Kufuatia taarifa ya serikali ya Tanzania iliyotolewa Januari 28 kuhusu madai yasiyo na msingi ya kuwepo kwa machafuko nchini Tanzania yaliyotolewa na Shirika la ndege la Uholanzi KLM, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Tanzania Prof Makame Mbarawa amepokea taarifa kutoka kwa meneja wa shirika hilo nchini Tanzania Bw. Alexander Van de Wint likiomba radhi. Mbali na taarifa hiyo ya kuomba radhi, KLM imemuarifu waziri kwamba imerejesha mara moja safari zake za ndege, ambapo safari zake za Dar es Salaam na Kilimanjaro zitaanza leo Januari 30.

Wakati huohuo licha ya kwamba KLM imeiomba radhi Kenya baada ya kutoa taarifa za kuwepo machafuko, Kenya itawasilisha malalamishi rasmi kwa Uholanzi baada ya shirika la ndege la Uholanzi KLM kutangaza kusitisha safari zake kwa sababu ya hofu ya ‘machafuko’ nchini Kenya na Tanzania.

Ingawa madai hayo dhidi ya Kenya baadaye yaliondolewa kwenye tovuti ya shirika la ndege la KLM, Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen alisema Kenya, ambayo tangu wakati huo iliwasiliana na mwakilishi wa nchi wa KLM, bado inadai kutaka kuonana na Uholanzi kwa kile alichosema ni taarifa za uongo, za kupotosha na hazina msingi wowote.