Rais wa Afrika Kusini asema msukosuko wa umeme unaendelea kutatiza ongezeko la uchumi
2023-01-30 08:27:23| CRI

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema msukosuko wa umeme unaoendelea kuikumba Afrika Kusini unaathiri ongezeko la uchumi na uwekezaji.

Akiongea jana kwenye mkutano wa kamati kuu ya utendaji ya chama tawala cha nchi hiyo ANC, Rais Ramaphosa amesema kukatika kwa umeme kunaathiri biashara, kusumbua kaya na kukwamisha utoaji wa huduma za jamii, na kwamba kuondoa msukosuko wa nishati nchini Afrika Kusini ni moja ya mambo ya haraka na muhimu.

Amesema kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme makampuni yamekuwa yanasita kuwekeza, uzalishaji umepungua, ongezeko la uchumi si endelevu na nafasi za ajira haziwezi kuongezwa kwa kiwango kinachotakiwa.

Amesema kwa sasa wamesaini makubaliaono na mashirika binafsi 26 yanayozalisha nishati endelevu ili kuzalisha megawati 2,800, na pia wanajadili kuagiza megawati 1,000 kutoka kwa nchi jirani.