Tume ya pamoja yaripoti ishara nzuri kuhusu haki za wanawake nchini Afghanistan
2023-01-31 19:39:14| cri

Tume ya Kamati Kuu ya Mashirika nchini Afghanistan imeripoti kuwa na ishara nzuri kuhusu haki za wanawake nchini humo.

Tume hiyo ilipelekwa nchini Afghanistan wiki iliyopita kuangalia athari za marufuku yaliyotangazwa na Taliban Disemba 24, 2022 ya kuwazuia wanawake kufanya kazi katika mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka ndani na nje ya nchi hiyo, pamoja na kazi za kibinadamu. Siku chache baada ya tangazo hilo, Wizara ya Afya ya Umma nchini Afghanistan ilisema agizo hilo halitahusu sekta ya afya na wizara ya elimu.

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu Martin Griffiths aliyeongoza tume hiyo kwenda nchini Afghanistan amesema, licha ya kuweka wazi wasiwasi wao kuhusu amri hiyo, walipendekeza kuongezwa maeneo ambayo hayataguswa na uamuzi huo. Ameongeza kuwa, kutokana na hilo, walilazimika kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi tisa wa Taliban, akiwemo kaimu waziri wa mambo ya nje, kaimu waziri wa uchumi na manaibu wawili wa waziri mkuu wa nchi hiyo pamoja na waziri wa mambo ya ndani.