Iran yalaani kauli za vitisho zilizotolewa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani
2023-01-31 17:38:28| cri

Iran imeionya Marekani kuwa haitavumilia uchochezi wowote dhidi ya mamlaka na maslahi yake, na itajibu ipasavyo kile ilichokiita kauli za vitisho zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken ambaye yuko ziarani Mashariki ya Kati.

Onyo hilo limetolewa na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kanaani, siku moja baada ya Bw. Blinken kuzungumza katika televisheni ya Kiarabu ya Al Arabiya kuwa maamuzi yote yako mezani endapo mazungumzo ya kufufua Makubaliano ya Nyuklia ya Iran ya mwaka 2015 yatashindwa kupata matokeo mazuri. Alisema serikali ya Marekani haiondoi uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia.

Kanaani pia ameionya serikali ya Marekani kuhusu majukumu ya kisheria na kimataifa ya kauli zake za vitisho dhidi ya Iran na matokeo ya kisiasa ya kauli hizo za uchochezi.