Kuneemeka kwa China ndio kuneemeka kwa nchi za Afrika
2023-02-02 15:26:47| CRI

Watu husema mwaka mpya huleta matumaini mapya. Lakini kwa uchumi wa dunia wa mwaka 2023, inahofiwa kuwa matarajio hayo sio mazuri sana, wasomi wengi wanakadiria kuwa kasi ya ukuaji uchumi itaendelea kupungua. Kwa Afrika haswa ukanda wa kusini mwa Sahara, watu wanaendelea kulalamikia bei kubwa ya bidhaa kutokana na athari za janga la COVID-19, mgogoro kati ya Russia na Ukraine pamoja na Marekani kuchukua hatua kali za kushughulikia mfumuko mkubwa wa bei ndani ya nchi.

Lakini, Umoja wa Mataifa na taasisi kadhaa za utafiti hivi karibuni zimeongeza tena na tena makadirio yao kuhusu ukuaji wa uchumi wa China kwa mwaka 2023. Hii ni habari njema sio kwa China tu bali hata kwa dunia, na hususan barani Afrika. Benki ya Maendeleo ya Afrika nayo pia imesema ukuaji wa Afrika mwaka huu utakuwa juu ya 4% ikilinganishwa na ilivyovyokadiriwa awali, na China ndio sababu kuu ya ongezeko hilo. Kwa hivyo, wakati uchumi wa dunia unaendelea kukua polepole, kuimarika kwa uchumi wa China kutainufaisha vipi Afrika?

Mwaka jana, kiwango cha biashara kati ya China na Afrika kilitarajiwa kuzidi dola za kimarekani bilioni 260, na kwa mara nyingine tena thamani ya bidhaa zilizoagizwa na China kutoka Afrika ilizidi ile ya mauzo ya kwenda Afrika. Wakati China ikitoa kipaumbele kwa kuchochea mahitaji ya ndani mwaka 2023, nguvu ya matumizi ya watu wa China itaongezeka, na bila shaka uagizaji wa bidhaa za Afrika utaendelea kukua. Wakati huo huo, ukuaji wa uchumi wa China unatarajiwa kuchochea ukuaji wa jumla wa Asia. Kama soko muhimu la bidhaa za Afrika, Asia inachukua takriban 40% ya jumla ya mauzo ya bidhaa za Afrika. Wakati huohuo, baada ya China kufungua tena mipaka yake, wafanyabiashara wadogo wa Afrika wanaweza kuja China kwa urahisi na kuleta idadi kubwa ya bidhaa bora lakini zenye bei nafuu kwa watu wa Afrika, na kupunguza gharama ya maisha kwa watu wa kawaida.

Pili, China itafanya ushirikiano mkubwa zaidi na Afrika, na watu wa Afrika watashuhudia miradi mingi zaidi ya kuboresha maisha yao. Katika miaka ya hivi karibuni, kupitia pendekezo la "Ukanda Mmoja, Njia Moja” na Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, barabara mpya, viwanja vya ndege vipya, hospitali mpya zimejitokeza katika nchi za Afrika, na kurahisisha maisha ya watu wa kawaida. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na AidData, maabara ya utafiti yenye makao yake makuu katika Taasisi ya Utafiti ya William & Mary nchini Marekani, miradi ya maendeleo ya ushirikiano kati ya China na Afrika ni muhimu katika kupunguza ukosefu wa usawa wa watu wa Afrika.

Tatu, hivi karibuni, Misri, Kenya na Afrika Kusini zimechaguliwa kuwa nchi za kwanza kupokea vikundi vya watalii vya China, karibu miaka mitatu baada ya China kusimamisha safari za nje kutokana na janga la COVID-19. Sekta ya utalii inachangia takriban asilimia 10 ya pato la taifa la Afrika. Janga hili la miaka mitatu limesababisha kushuka kwa zaidi ya asilimia 80 ya watalii wa kimataifa wanaokuja Afrika. Kama nchi inayotoa chachu kubwa katika sekta ya utalii duniani, China ni chanzo muhimu cha watalii barani Afrika. Sasa watu wa China wanaweza kusafiri nje ya nchi, jambo ambalo litakuza ufufuaji na maendeleo ya utalii katika nchi za Afrika.

Waswahili husema, “Ukikaa karibu na muwaridi lazima utanukia”. Wakati kuna sintonfahamu duniani, tunapaswa kuchagua matumaini. Mwaka 2023 unaadhimisha miaka 10 tangu Rais Xi Jinping wa China kuweka mbele dhana ya sera ya " Udhati, Nia njema, Upendo, Matokeo Halisi " na maana halisi ya sera ya Afrika ya mtazamo wa haki na faida. Haijalishi kwa mtazamo wa historia, hali halisi ya sasa au siku zijazo, Afrika inapaswa kuweza kutumia fursa zinazotokana na kufufuka kwa uchumi wa China na kupanua zaidi ushirikiano. Sio tu katika suala la maendeleo ya uchumi tu, bali pia nyanja za siasa na utamaduni, waafrika wenzangu tutafaidika kutokana na kuimarishwa kwa uhusiano kati ya pande hizo mbili.