Mwanadiplomasia mwandamizi wa China akutana na rais wa UNGA
2023-02-03 14:36:55| CRI

Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamati ya Mambo ya Nje ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Wang Yi amekutana na rais wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa Csaba Korosi jana hapa Beijing.

Katika mazungumzo yao, Wang Yi amesema dunia ya sasa inakabiliwa na ukosefu wa utulivu na amani, na kuzitaka nchi zote kupeperusha bendera ya Umoja wa Mataifa na kufanya kazi kwa pamoja ili kupunguza idadi ya vurugu za siasa za kijiografia duniani, kupunguza chuki na mabavu, na kufanya zaidi majadiliano, mashauriano na ushirikiano wa kimataifa.

Amesema China iko tayari kuimarisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa kutekeleza zaidi Pendekezo la Maendeleo ya Dunia na Pendekezo la Usalama wa Dunia, na kwa pamoja kukabiliana na changamoto za dunia kama vyanzo vya maji na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Bw. Korosi amesema Umoja wa Mataifa unatumai kuimarisha ushirikiano na China, kwa pamoja kushinda janga la COVID-19, kukabiliana na changamoto za dunia na kuhimiza utimizaji wa Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya Mwaka 2030.