Viongozi wa Afrika watakiwa kutoa tena ahadi ya dhamira ya kutokomeza UKIMWI kwa watoto kabla ya mwaka 2030
2023-02-03 08:40:52| CRI

Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Philip Mpango amewataka viongozi wa nchi za Afrika kuonyesha uongozi wao kwa kutoa tena ahadi ya dhamira ya kutokomeza UKIMWI kwa watoto kabla ya mwaka 2030.

Akiongea mjini Dar es salaam kwenye mkutano wa mawaziri wa afya wa nchi wanachama wa Umoja wa kutokomeza UKIMWI kwa watoto kabla ya mwaka 2030, Dk. Mpango amezitaka nchi za Afrika zisibweteke kwani mwaka 2030 unakaribia.

Dk. Mpango pia ameushukuru mpango wa pamoja wa Umoja wa mataifa chini ya Shirika la kupambana na UKIMWI la Umoja wa mataifa (UNAIDS), Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), Shirika la afya duniani (WHO) na wadau wengine wa kimataifa kwa kuanzisha mpango huo unaoziba pengo lililo wazi kwenye mapambano dhidi ya UKIMWI.

Nchi 12 za Afrika (Angola, Cameroon, Cote d’Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Msumbiji, Nigeria, Afrika Kusini, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe) ni wanachama wa umoja huo.