Hatua kali za ulinzi wa mazingira nchini Uganda zaonyesha mafanikio
2023-02-03 08:41:46| CRI

Wakati dunia inaadhimisha siku ya ardhi oevu, Uganda imesema hatua zake kali za ulinzi wa mazingira zimeanza kuwa na matokeo chanya.

Waziri wa nchi anayeshughulikia suala la mazingira Bibi Beatrice Anywar amesema kwenye taarifa iliyotolewa mjini Kampala, kuwa Uganda sasa imeweza kurudisha baadhi ya maeneo yaliyovia ya ardhi oevu.

Amesema maeneo ya ardhi oevu nchini Uganda yamekuwa yakipungua kutoka asilimia 15.6 ya mwaka 1996 hadi asilimia 13 ya mwaka 2015, huku asilimia 8.9 tu kati ya hizo zikiwa salama na 4.1 zikiwa zimeharibiwa. Lakini kutokana na hatua zilizochukuliwa na serikali ya Uganda eneo la asilimia 4.1 limerudisha katika hali ya asili.

Mbali na hatua za kupiga marufuku kutoa vibali kwenye maeneo ya ardhi oevu na kuwa na kikosi cha polisi wa ulinzi wa mazingira, hatua nyingine zilizochukuliwa na serikali ni pamoja na kuanzisha programu za kurudisha maeneo ya ardhi oevu, kuweka mipaka kwenye maeneo hayo, usimamizi na kuongeza mwamko wa umma.