Wadau wa elimu wa Afrika Mashariki wataka mfumo endelevu elimu
2023-02-06 23:35:42| cri

Wadau wa elimu katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda wamekubaliana kuwa, ipo haja ya nchi hizo kutengeneza mifumo himilivu ya elimu ili ufundishaji uendelee pindi yanapotokea majanga.

Uamuzi huo ni miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa katika mkutano uliohusisha nchi hizo ulioandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Elimu Afrika Mashariki ya Aga Khan (AKU-IED EA) uliofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Akisoma tamko la pamoja lililoandaliwa na wadau wa elimu katika nchi zote tatu, Mkurugenzi wa elimu maalum Tanzania Dk Magreth Matonya amesema, wamekubaliana kuwekeza katika teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA). Amesema nchi zote tatu zimeona umuhimu wa tehama katika elimu wakati wa majanga, hivyo uwekezaji mkubwa unapaswa kufanyika kwenye eneo hilo ili kuwezesha elimu kuendelea kutolewa.