Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania imeweka zuio la matumizi ya vitabu visivyo na maadili ya kitanzania mashuleni ili kuendelea kusimamia utoaji wa elimu na kuhakikisha njia mbalimbali za ufundishaji zinazingatia ubora na maslahi ya nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Francis Michael amesema, kumekuwa na shule ambazo zinaingiza nchini vitabu ambavyo maudhui yake hayaendani na mila, desturi na utamaduni wa kitanzania.
Pia Dkt. Francis amewakumbusha wamiliki wa shule nchini humo kuzingatia sheria na taratibu, na kuhakikisha wanatumia vitabu vya kiada na ziada ambavyo vinafuata miongozo ya kitanzania, na kama hawatafanya hivyo, adhabu kali zitatolewa ikiwemo kuzifungia na kuzifutia usajili shule husika.