Viongozi wa Afrika Mashariki wametoa wito wa kusitishwa mapigano mara moja katika mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Hayo yamo kwenye taarifa iliyotolewa na Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika mji mkuu wa kibiashara wa Burundi Bujumbura siku ya Jumamosi ili kutathmini hali ya sasa ya usalama katika mashariki ya DRC.
Taarifa imewaelekeza wakuu wa vikosi vya ulinzi kukutana ndani ya wiki moja ili kuweka muda mpya wa kujiondoa.
Mkutano huo pia umependekeza nchi zinazochangia wanajeshi kupeleka wanajeshi mara moja na kuitaka DRC kuwezesha kutumwa kwa wanajeshi kutoka Sudan Kusini na Uganda.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa lilirejea tena wito wake kwa kundi la waasi la M23 kuondoka katika maeneo yote wanayoyakalia nchini DRC na kutaka makundi yote yenye silaha kunyang’anywa silaha.