Zanzibar kuandaa maonesho ya kusafiri ili kutangaza utalii wa kimazingira
2023-02-06 10:30:04| CRI

Zanzibar wiki hii inatarajiwa kuandaa Maonesho ya Uwekezaji na Usafiri wa Utalii, yakiwa na lengo la kutangaza utalii wa kimazingira kwa kusimamia kwa ufanisi na kuhifadhi utamaduni wa Zanzibar, rasilimali za kimazingira na za kihistoria.

Akifafanua kuhusu maonesho hayo Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Rahim Bhaloo amesema kaulimbiu ya maonesho hayo yatakayofanyika Februari 9 hadi 11 ni “Zanzibar ya Kijani”.

Kwa mujibu wa Bw. Bhaloo maonesho hayo yatafunguliwa na rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi katika viwanja wa Mnazi Mmoja Unguja. Maonesho hayo ya siku tatu pia yatajumuisha mazungumzo ya wadau wa utalii, kongamano la uwekezaji wa utalii, warsha mbalimbali na majadiliano ya jopo.

Amesema kaulimbiu “Zanzibar ya Kijani” inatoa wito wa utalii unaohusisha uwekezaji wa kimkakati, shughuli endelevu za biashara na machaguo ya usafiri yanayowajibika.