Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) imelaani vurugu zilizotokea tarehe 2 mwezi Februari katika kaunti ya Kajo-Keji jimboni Central Equatoria nchini Sudan Kusini, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 27 na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Mwakilishi maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini Bw. Nicholas Haysom alitoa wito kwa mamlaka husika kuanza uchunguzi haraka iwezekanavyo na kuwafikisha wanaohusika mbele ya sheria.
Haysom alitoa taarifa mjini Juba akisema vurugu hizo ni jambo lisilokubalika, na zinakwenda kinyume na ujumbe uliotolewa kwenye ziara ya amani ya “Ecumenical Peace Pilgrimage” kwa Sudan Kusini, inayotoa wito wa amani na maafikiano. Aliongeza kuwa watu wasiopungua elfu mbili wamekuwa wakimbizi, na wengi wao ni wanawake na watoto.