Wanawake wanaendelea kuchangia mapato ya nchi kwa kiasi kikubwa kwa kujihusisha na shughuli mbalimbali zikiwemo kazi za kwenye makampuni, sekta ya umma na sekta isiyo kuwa rasmi ambayo ndiyo inayowapatia ajira nyingi zaidi wanawake ikiwemo mama lishe, ujasiriamali na biashara nyingine tofauti zinazosaidia kusukuma maendeleo ya familia zao na taifa kwa ujumla.
Mama ntilie au mama lishe ni watu muhimu sana katika jamii mbalimbali, kwani wao ndio wanawaokoa wafanyakazi, wafanyabiashara, au hata watu wengine mbalimbali kwa mapishi yao, wakiwa kwenye harakati zao za kazi au biashara. Biashara hii ya mama ntilie ni moja ya kazi inayowasaidia wanawake wengi kupanua wigo wa uchumi. Na biashara hii inashikiliwa na idadi kubwa ya wanawake kuliko wanaume, ama tunaweza kusema wanashikilia ustawi wa afya za watu wengi mijini. Hivyo leo hii katika kipindi cha ukumbi wa wanawake tutaangazia wanawake wanaojishughulisha na biashara ya mama ntilie au mama lishe jinsi wanavyochangia mapato ya nchi.