Naibu rais wa Kenya Rigathi Gachagua amesema kuwa serikali inaongeza juhudi kudhibiti ongezeko la maambukizi mapya ya UKIMWI kwa vijana.
Akizungumza alipokutana na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS) mjini Nairobi, Gachagua amesema serikali imewahusisha wakuu wa mikoa, wabunge na vikundi husika katika kupambana na matishio matatu yanayowakabili vijana, ambayo ni maambukizi ya VVU, mimba za utotoni na ukatili wa kingono na kijinsia.
Kutokana na ripoti ya Kamati ya Taifa ya Udhibiti wa Magonjwa ya Mlipuko ya mwaka 2022, karibu asilimia 52 ya maambukizi mapya 29,380 yalikuwa kati ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 – 29, huku nyingi ya kesi hizo zikiwa ni watoto wa kike na wasichana.
Gachagua amesema idadi kubwa ya maambukizi kwa mwaka 2021 ilitokana na mlipuko wa janga la COVID-19, ambapo kutokana na kufungwa kwa shule, watoto walikuwa nyumbani na hivyo kuwa hatarini zaidi kufanyiwa ukatili wa kingono, ukeketaji, na ndoa za lazima, mambo yanayohusishwa na kuongezeka kwa idadi ya maambukizi.