Serikali ya Tanzania imetoa zaidi ya Sh2.7 bilioni kwa ajili ya kusambaza nishati ya umeme kwenye maeneo ya migodi ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu wilayani Chunya, mkoani Mbeya.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera wakati akitoa taarifa ya kuanza kwa maonyesho ya teknolojia ya madini na fursa za uwekezaji yanayotarajia kufanyika wilayani Chunya Februari 21 hadi 25 mwaka huu, ambayo yatatumika kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.
Amesema kupitia maonyesho hayo, serikali imetoa fursa kwa wawekezaji wakubwa na wa kati kushiriki kikamilifu ili kuona teknolojia za uwekezaji katika sekta ya madini kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali.