Guterres ahuzunishwa na idadi kubwa ya vifo nchini Uturuki na Syria kutokana na tetemeko kubwa la ardhi
2023-02-07 09:34:30| CRI

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres ameelezea masikitiko yake makubwa baada ya watu wengi kupoteza maisha kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria.

Bw. Guterres amesisitiza dhamira ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia, akiongeza kuwa timu za Umoja wa Mataifa zimeshafika kutathmini mahitaji na kutoa msaada. Amesema wanaitegemea jumuiya ya kimataifa kusaidia maelfu ya familia zilizokumbwa na janga hili, wengi wao wakiwa tayari wanahitaji zaidi misaada ya kibinadamu katika maeneo ambayo kuyafikia ni changamoto.

Wakati huohuo Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Bw. Moussa Faki Mahamat ameeleza kuwa Afrika inashikamana na Uturuki na Syria kufuatia matetemeko makubwa ya ardhi katika nchi hizo mbili.