Kampuni ya Bandari na Reli ya Msumbiji (CFM) imetangaza kuwa, treni ya kwanza iliyosafirisha bidhaa kwa ajili ya ujenzi wa reli nchini Malawi imefanya safari ya kwanza rasmi ya reli kutoka Nova da Fronteira, katikati ya nchi hiyo hadi nchini Malawi kwa mafanikio.
Treni hiyo iliyobeba saruji, ambayo ni mali ya kampuni ya China inayowajibika na ukarabati wa njia ya reli nchini Malawi, iliondoka katika bandari ya Beira ijumaa iliyopita.
Shirika la Habari la Msumbiji (AIM) limemnukuu mkurugenzi wa CFM Bonaventura Mahave akisema, kuwa njia hiyo ya reli kati ya nchi hizo mbili iliacha kutumika mwaka 1986 kufuatia vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa miaka 16 nchini humo.
Habari zinasema, njia hiyo ya reli inatarajiwa kupunguza msongamano mkubwa katika mtandao wa barabara kati ya Beira na Malawi, na pia kuwa na ushindani na njia ya reli inayounga Malawi na bandari ya Nacala iliyoko kaskazini mwa Msumbiji.