Vifo vya watoto chini ya miaka mitano vyapungua hadi 43 kwenye 1000 mwaka 2022
2023-02-08 10:07:08| CRI

Mamlaka za afya Tanzania zimesema vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano vimepungua kutoka 67 kwenye 1000 mwaka 2016 hadi 43 kwenye 1000 mwaka 2022.

Akitangaza takwimu mpya kwenye ripoti ya viashiria vya afya ya watoto na malaria ya mwaka 2022 mjini Dodoma, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema hii ni hatua kubwa kwa serikali kwenye masuala ya afya. Amefafanua kuwa mpango wa maendelo ya taifa unalenga kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano hadi 40 kwenye 1000 kufikia mwaka 2025, na kusema lengo hilo litatimizwa kutokana na juhudi zinazofanywa na serikali kuboresha sekta ya afya na kilimo ambazo zinachangia pakubwa kwenye usalama wa chakula.

Waziri huyo amesema Tanzania inakadiriwa kupunguza kiwango cha vifo vya watoto chini ya miaka mitano hadi 25 kwenye 1000 kufikia 2030 kama ilivyo kwenye malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa.