Idadi ya vifo vilivyotokana na tetemeko la ardhi nchini Uturuki na Syria yafikia zaidi ya 7,700
2023-02-08 10:23:00| CRI

Idadi ya vifo vilivyotokana na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea Jumatatu imefikia zaidi ya 7,700 nchini Uturuki na Syria hadi jana, huku wito ukitolewa kuondoa vikwazo vya Marekani dhidi ya Syria.

Idadi ya vifo katika nchi zote mbili inatazamiwa kuongezeka zaidi huku shughuli za uokoaji zikitatizwa na hali mbaya ya hewa. Mkoa wa Hatay, kusini mwa Uturuki na mji wa Aleppo, kaskazini mwa Syria umeshuhudia vifo vya watu wengi zaidi.

Huko nchini Syria, Wizara ya Mambo ya Nje jana ilikosoa vikwazo vya Marekani kwa kuzuia kazi za kibinadamu na shughuli za uokoaji katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita. Katika taarifa yake, wizara hiyo ilisema Wasyria, wakati wakikabiliana na janga la tetemeko la ardhi, wanachimba vifusi kwa mikono yao wenyewe au kwa kutumia zana rahisi zaidi kwani vifaa vya kuondoa vifusi hivyo vimepigwa marufuku kutokana na vikwazo vya Marekani.

Habari nyingine zinasema timu ya uokoaji ya China jana alasiri iliondoka Beijing kuelekea Uturuki kwa ndege ya kukodi ili kujiunga na juhudi za kutoa misaada kufuatia tetemeko la ardhi nchini humo. Timu hiyo yenye watu 82 ilitumwa na Wizara ya Usimamizi wa Hali ya Dharura ya China kwa ombi la serikali ya Uturuki.