Sudan imetoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuondoa vikwazo lilivyoiwekea nchi hiyo tangu mwaka 2005.
Ombi hilo lilitolewa na kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ali Al-Sadiq alipokutana na mabalozi wa nchi wajumbe wa kudumu na wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama. Bw. Al-Sadiq amesema kuwa Sudan inadai kukomeshwa kwa vikwazo ilivyowekewa chini ya azimio nambari 1591 la Baraza la Usalama la mwaka 2005, akisisitiza kuwa hali ya Sudan ya leo ni tofauti kabisa na ilivyokuwa mwaka 2005 wakati vikwazo vilipowekwa.
Ameongeza kuwa maendeleo ya sasa nchini Sudan yanailazimu jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi za vyama vya Sudan kuelekea kwenye mpito wa demokrasia, na kuondolewa kwa vikwazo.
Bw. Al-Sadiq ameendelea kuwataka mabalozi hao kuzifahamisha serikali zao kuhusu msimamo wa Sudan, akitumai kuwa msimamo huo utaungwa mkono wakati suala hilo litakapojadiliwa katika Baraza la Usalama.
Vikwazo ilivyowekewa Sudan ni pamoja na vya silaha, marufuku ya kusafiri, na kuzuiwa kwa mali za watu wanaohusika katika mgogoro wa Darfur.