Idadi ya vifo kwenye tetemeko la ardhi Uturuki na Syria yafikia 12,000
2023-02-09 10:12:06| CRI

Idadi ya watu waliofariki kutokana na matetemeko mabaya ya ardhi yaliyotokea Jumatatu nchini Uturuki na Syria imepita 12,000, huku uwezekano wa kupata manusura zaidi katika hali ya hewa ya baridi ukiwa mdogo kabla ya muda muhimu wa saa 72 kuisha.

Waokoaji na watu waliojitolea wanafanya kazi usiku na mchana kutafuta watu walionasa kwenye vifusi huku kiwango cha watu wanaoweza kuishi bila chakula au maji kikishuka sana baada ya saa 72, ambayo inakaribia kwa kasi.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, timu za utafutaji na uokoaji kutoka zaidi ya nchi 65 zimewasili katika maeneo ya tetemeko la ardhi nchini Uturuki kutoa msaada katika juhudi za kukabiliana na tetemeko hilo.

Ndege iliyokuwa imebeba timu ya uokoaji ya watu 83 kutoka China na tani 20 za vifaa iliwasili katika mji wa Adana kusini mwa Uturuki mapema Jumatano. Mbali na vifaa vya utafutaji na uokoaji, vya mawasiliano na matibabu, pia walileta mbwa wanne wa uokoaji.