China yatoa msaada wenye thamani ya dola milioni 4.42 kwa Syria
2023-02-09 10:08:18| CRI

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning amesema China itatoa msaada wa dharura wa kibinadamu wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 4.42 kwa Syria, ambao unajumuisha msaada wa dola za kimarekani milioni 2 na vifaa vya uokoaji vinavyohitajika sasa katika nchi hiyo iliyokumbwa na tetemeko kubwa la ardhi.

China pia inaharakisha utekelezaji wa mpango unaoendelea wa msaada wa chakula, ambapo tani 220 za ngano ziko njiani kuelekea Syria, na tani 3,000 zilizosalia za mchele na ngano zitasafirishwa kwa awamu mbili katika siku za hivi karibuni.

Wakati huohuo, Mao ametoa wito kwa Marekani kusimamisha mara moja vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Syria ili kutandika njia kwa kazi za uokoaji za kibinadamu.

Amesema Marekani imekuwa ikiingilia kati mgogoro wa Syria kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na njia ya kijeshi, kuweka vikwazo vikali vya kiuchumi, na kusababisha vifo na majeruhi wengi nchini humo. Hadi leo, jeshi la Marekani bado linashikilia maeneo makuu ya uzalishaji wa mafuta nchini Syria, likipora zaidi ya 80% ya mafuta yanayozalishwa, kufanya magendo na kuchoma hifadhi ya chakula ya Syria, na kusababisha mgogoro wa kibinadamu kuwa mbaya zaidi.