Vikwazo vya Marekani dhidi ya Syria vyatakiwa kuondolewa kufuatia tetemeko kubwa la ardhi kuikumba nchi hiyo
2023-02-09 15:05:34| cri

Tarehe 6, matetemeko makubwa ya ardhi yenye nguvu ya 7.8 kwenye kipimo cha Richter yalitokea kwenye maeneo ya kusini mashariki mwa Uturuki yanayopakana na Syria. Kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa na Wizara ya Afya ya Syria, matetemeko hayo yamesababisha vifo vya watu 1,250 na wengine 2,054 kujeruhiwa kwenye maeneo yanayodhibitiwa na serikali ya Syria, na huenda idadi hiyo ikaongezeka zaidi. Katika mji wa Allepo pekee, majengo yapatayo 50 yameanguka kutokana na matetemeko hayo.

Katika hali hiyo ya dharura, mashirika mbalimbali yakiwemo Shirika la Hilali Nyekundu la Syria na Kamati ya kupambana na ubaguzi wa rangi ya Marekani na nchi za kiarabu, yametoa wito kwa Marekani na nchi nyingine za magharibi kuondoa mara moja vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Syria, ili kuepusha hali ya kibinadamu kuwa mbaya zaidi. Lakini msemaji wa Wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price ameweka wazi kwamba Marekani itatoa misaada kupitia “washirika wake wa kibinadamu” tu, na imekataa kuwasiliana na serikali ya Syria.

Kutokana na janga hilo kubwa, wale wanasiasa wa Marekani wanaopiga kelele za “haki za kibinadamu” kila mara, wanapaswa kuonyesha huruma na uungaji mkono kwa watu wa Mashariki ya Kati kwa vitendo halisi, na kuondoa vikwazo mara moja dhidi ya Syria, ili kuwezesha misaada ya kibinadamu kuwafikia wenye mahitaji.