Uganda imesema haitaongeza tena makubaliano na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) baada ya kufanya kazi nayo kwa miaka 17.
Barua iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda kwa OHCHR, ya tarehe 3 Februari ambayo imetangazwa hadharani Jumanne, imesema kuwa ofisi hiyo sasa sio muhimu tena kwa kuwa hali ya haki za binadamu nchini Uganda imeboreka sana.
Kwa mujibu wa barua, kutokana na dhamira kubwa ya kuhimiza na kulinda haki za binadamu, kupata amani katika nchi nzima, pamoja na kuwa na taasisi imara za taifa za haki za binadamu na asasi za kijamii, nchi hiyo imeamua kutoongeza tena mamlaka ya OHCHR nchini humo.
Hata hivyo wizara imesisitiza kuwa Uganda itaendelea kushirikiana na makao makuu ya OHCHR, iwe moja kwa moja ama kupitia Tume ya Kudumu iliyopo Geneva.